JOPO la masheikh na wanasheria Waislamu, limebainisha hoja tatu muhimu ambazo ni sehemu ya hoja zitakazorudishwa serikalini, kufanyiwa kazi zaidi kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa jopo hilo lenye wajumbe 25, Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Shaabani Simba, kabla ya kubainisha hoja hizo, walipokea na kujadili mapendekezo kuhusu namna ya uanzishwaji wa mahakam hiyo nchini.
Mufti ambaye aliitisha mkutano mfupi na waandishi wa habari katika Ofisi za Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) jana, alisema mapendekezo hayo yalipelekwa kwao kutoka katika kikao cha Sekretarieti ya Serikali na Waislamu.
“Jopo la masheikh na wanasheria Waislamu la kurejesha Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara, limekutana kuanzia Julai 3 hadi 4, 2010 kupitia na kujadili mapendekezo ya Sekretarieti ya pamoja, kati ya Serikali na masheikh.
“Jopo lilijadili kwa kina na kuona kwamba kuna baadhi ya mambo muhimu ambayo bado yanahitaji kukaa tena na Serikali ili kufikia muafaka wa uendeshaji wa mahakama hiyo,” alisema Sheikh Simba.
Kati ya mambo hayo ambayo masheikh hao wanataka kujadili upya na Serikali, Sheikh Simba alitaja hoja inayohusiana na gharama za uendeshaji wa mahakama hiyo na namna uamuzi wa mahakama hiyo utakavyokuwa na nguvu ya kisheria.
Hoja nyingine ya tatu iliyotajwa na Sheikh Simba inahusu jinsi Mahakama ya Kadhi, itakavyoingizwa katika mfumo wa mahakama nchini.
No comments:
Post a Comment