Saturday, August 14, 2010

Mchungaji adaiwa kuomba rushwa ya ngono kizimbani Iringa!

MCHUNGAJI Michael Ngilangwa (35) ambaye pia ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Pomerin, wilayani Kilolo mkoani Iringa jana alipandishwa kizimbani kusomewa mashitaka ya kumuomba mwanafunzi rushwa ya ngono. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) inamtuhumu mchungaji huyo kuwa alimuomba rushwa ya ngono mwanafunzi wake wa kidato cha kwanza ili amsaidie kujua soma la Kingereza. Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu ya Mkoa wa Iringa, Martha Ngaze, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru mkoani hapa, Imani Nitume alisema Ngilangwa ni mwajiriwa wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) dayosisi ya Iringa. Alisema pamoja na kuomba rushwa ya ngono, Ngilangwa anatuhumiwa kutaka kumbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14 na hivyo kufanya jumla ya makosa yake kuwa mawili. Alisema Ngilangwa anashitakiwa kuvunja kifungu cha 25 cha sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika tukio hilo lililotokea Agosti 11 mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni ya Wihanzi, mjini Iringa. Alisema Ngilangwa akiwa na mwanafunzi huyo wakiwa katika nyumba hiyo ya wageni, aliomba rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi huyo kwa ahadi kwamba atamsaidia somo la Kiingereza na Bibilia ikiwa ni pamoja na kumpatia mahitaji yake mengine madogo madogo akiwa shuleni hapo. Mtuhumiwa huyo alikana mashikata yote mawili ambayo ushahidi wake haujakamilika kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka huyo wa Takukuru. Hata hivyo Mwendesha Mashitaka huyo alisema dhamana kwa mtuhumiwa ipo wazi kwa kuzingatia masharti yaliyotolewa na mahakama hiyo. Akisoma masharti ya dhamana kwa mtuhumiwa huyo, Hakimu Ngaze alisema kuwa ili mtuhumiwa huyo aweze kudhaminiwa anapaswa kuwa na wadhamini wawili mmoja awe mkazi wa Manispaa ya Iringa na wa pili awe mtumishi wa serikali ambao watasaini dhamana ya shilingi milioni 2. Hata hivyo mshitakiwa huyo aliiambia Mahakama hiyo kuwa, ana wadhamini wawili ambao pamoja na kuitwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kuthibitisha udhamini wao hawakuwa na barua yoyote inayowatambulisha kama wao ni wadhamini hali iliyosababisha Hakimu huyo kumtaka mtuhumiwa huyo kwenda mahabusu hadi Agosti 26, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment