Tuesday, December 21, 2010

Yanga na Simba zawekwa mitegoni katika michezo ya CAF 2011.



SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) lilimeziweka mtegoni klabu za Simba na Yanga kwenye ratiba iliyopangwa jana jijini Cairo, Misri.

Wawakilishi hao wa Tanzania, Simba na Yanga zimepangwa kuanza kampeni yake dhidi ya wawakilishi wa Comoro na Ethiopia na kupewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa hatua ya kwanza.

Wakati Watanzania wenye furaha ya timu yao ya taifa Kilimanjaro Stars kutwaa Kombe la Chalenji baada ya miaka 16, sasa macho yake yanasubili mafanikio ya klabu hizo kongwe kwenye michuano ya Afrika.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Simba wataanza harakati zao za kutafuta ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini kwa kuikabili Elan Club de Mitsoudje ya Comoro.

Lakini, endapo itavuka kigingi hicho, Simba itakuwa na kibarua kigumu cha kuivua ubingwa TP Mazembe timu pekee ya Afrika iliyofanikiwa kutinga fainali za Klabu Bingwa ya Dunia baada ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa michezo hiyo, Jumamosi iliyopita na kufungwa na Inter Milan ya Italia kwa mabao 3-0.

Kutokana na ratiba hiyo TP Mazembe wamepewa nafasi kubwa ya kufuzu kwa fainali ya tatu kutokana na wapinzani wake hao wa kutoka Tanzanian au Comoro.

Miamba hiyo inayosifika kwa kutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani watakuwa wakimsubili mshindi kati ya Elan Club Mitsoudje au Simba.

Kwa upande wao, watani zao, Yanga ambao watacheza Kombe la CAF wataanza kucheza nyumbani dhidi ya Dedebit ya Ethiopia katika mchezo wa Januari 28 hadi 30 mwaka huu na marudiano Februari 11 hadi 13 mwakani.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa jana na CAF, endapo Yanga itaitoa timu hiyo ngeni na ambayo haifahamikivizuri (Dedebit), inaweza kukutana na mbaya wa Simba, Haras el Hodoud kutoka Misri.

El- Hodoud ndiyo timu ambayo mwaka jana iliitoa nishai Simba kwa mabao 5-1 katika mchezo wa marudiano nchini Misri baada ya awali kutoka sare kwa bao 1-1 katika mchezo wa awali jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi wa Zanzibar, Ocean View wanaoshiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo mikubwa barani Afrika, wamepangiwa dhidi ya AS Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

KMKM wa Zanzibar watakuwa wenyeji wa DCMP kutoka DR Congo katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika wakianzia nyumbani.

Kulingana na ratiba hiyo ya CAF, klabu kadhaa ambazo ni Al Ahly (Misri), Entente Setif (Algeria), Al- Itihad (Libya), Stade Malien (Mali), TP Mazembe (DRC ambao ni mabingwa watetezi), Al Hilal na El Mireikh (Sudan), Esperance (Tunisia ) na Dynamo ya Zimbabwe, zimefuzu kucheza raundi ya kwanza ya michuano hiyo kutokana na matokeo mazuri msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment