MWENYEKITI wa Yanga Iman Madega amesema hatambui kung’olewa kwake katika nafasi hiyo na ameliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumpatia ufafanuzi juu ya uhalali wake kama kiongozi wa klabu hiyo. Wanachama wa Yanga walimtoa Madega madarakani Jumapili katika mkutano mkuu wa kupitisha Katiba uliofanyika kwenye bwalo la Polisi Oysterbay, Dar es Salaam. Akizungumza Dar es Salaam jana, Madega alisema amepata mwongozo kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kwa mujibu wa Katiba yeye bado Mwenyekiti wa Klabu hiyo mpaka uchaguzi utakapofanyika. Katika mkutano huo, Madega alipendekeza uchaguzi ufanyike Julai 4 terehe ambayo ilipingwa na wanachama waliotaka uchaguzi ufanyike Juni 27. Madega alisema wanachama wachache ndio waliotamka kwamba wanataka uchaguzi wakati yeye alikuwa amekwishafunga mkutano, hivyo kitendo hicho ni kinyume na Katiba na kwamba ni ishara ya kuvuruga amani na utulivu ndani ya Yanga. “Katika barua yangu nimeiomba TFF inijulishe kama kuna uhalali wa kutolewa maamuzi ya aina yoyote baada ya Mwenyekiti wa kikao kufunga mkutano,”alisema Madega.
No comments:
Post a Comment